Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Moja ya mafundishi muhimu ya dini ya Uislamu ni kuishi vizuri na watu. Qur’ani Tukufu kuhusiana na thamani ya jambo hili inasema:
وَلَا تَسْتَوِی الْحَسَنَةُ وَلَا السَّیِّئَةُ ادْفَعْ بِالَّتِی هِیَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِی بَیْنَکَ وَبَیْنَهُ عَدَاوَةٌ کَأَنَّهُ وَلِیٌّ حَمِیمٌ
Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu. 1
Sherehe:
Kila kitendo chetu kwa hakika kinapaswa kuchukua rangi na harufu ya uongozi wa Mwenyezi Mungu. Mwanadamu hapaswi tu kuijaza nafsi yake nuru ya uongofu, bali pia kauli na matendo yake yawe sababu ya kuandaa mazingira ya uongofu kwa wengine. Hili haliwezekani isipokuwa kupitia urafiki na mapenzi.
Wakati mwingine, hujitokeza misukosuko kutoka kwa wengine dhidi yetu. Katika hali kama hizi, kuna njia mbili za kukabiliana nazo: Kwanza, kurejesha ubaya uliofanyiwa na wengine kwa ubaya, yaani kulipiza kisasi; pili, kujizuia na badala yake kuelekeza upendo kwao.
Kama ambavyo Imam Sadiq (a.s) amesema:
صِلْ مَنْ قَطَعَکَ وَاُعْفُ عَمَّنْ ظَلَمَکَ وَأَعْطِ مَنْ حَرَمَکَ وَ أَحْسِنْ إِلَی مَنْ أَسَاءَ إِلَیْکَ
Muunge yule aliyekukatia udugu, na msamehe yule aliyekudhulumu, na mpe yule aliyekunyima; na mtendee wema yule aliyekutendea ubaya. 2
Matunda ya mwenendo huu, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu katika aya iliyotajwa, ni kuzaliwa urafiki na mapenzi, yule ambaye muda mfupi uliopita alikuwa akidhihirisha uadui, anaweza akaathiriwa na matendo yetu, akabadilika na kuwa rafiki wa karibu ambaye mapenzi yake yote yameelekezwa kwetu, hapo ndipo ambapo mtu aliyepambwa kwa uongofu anakuwa na nafasi ya kuwaandaa wengine pia kuongoka, na kuwakalisha kwenye meza ya Mwenyezi Mungu.
Muamala wa Imam Hasan al-Mujtaba (a.s) na mtu kutoka Shamu:
Mtu mmoja kutoka Shamu alimwona Imam Hasan (a.s) akiwa amepanda kipando, akasimama mbele ya Imam na kuanza kumtukana, Imam alinyamaza, hakumjibu, alipomaliza matusi yake, Imam akamsalimia kwa amani, akatabasamu na kisha akasema:
Ewe mzee! Nadhania wewe ni mgeni! Inaonekana umekosea! Sasa, iwapo utatutaka radhi na msamaha, sisi tutakusamehe; na kama utatuomba kitu tutakupatia, na kama utahijaia kuongozwa sisi tutakuongoza, na kama utaomba kipando sisi tutakuachia, na kama una njaa sisi tutakupatia chakula, na kama hauna mavazi basi sisi tutakuvisha, na kama una haja yeyote basi sisi tutakutimizia, na ikiwa umefukuzwa kwenu kwenu sisi tutakupokea, ukiwa na haja yoyote sisi tutakuhudumia.
Kwa sasa ni bora zaidi ulete mizigo yako nyumbani kwetu na ukae nasi hadi safari yako itakapomalizika, kwani nyumba yetu ni kubwa na yenye kila aina ya starehe na faraja....
Wakati yule mtu wa Shamu aliposikia maneno haya ya huruma kutoka kwa Imam, alianza kulia na kusema:
Nashuhudia kuwa wewe ndiye Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake, hakika Mwenyezi Mungu anajua vyema wapi aiweke risala yake, hapo kabla, wewe na baba yako mlikuwa ni miongoni mwa viumbe wa Mungu ninao wachukia zaidi, lakini sasa hakuna ninayempenda zaidi yenu. 3
Baada ya hayo, mtu huyo akahamishia mizigo yake nyumbani kwa Imam na akawa mgeni wake mpaka alipoondoka Madina, kuanzia hapo, akawa miongoni mwa waliokuwa na itikadi ya kuwapenda watu wa nyumba hii tukufu.
Rejea:
1. Surah Fussilat, Aya ya 34.
2. Bihar al-Anwar, Juz. 68, Uk. 423.
3. Manāqib Āl Abī Ṭālib, Juz. 4, Uk. 19, Kisa cha Mzee kutoka Sham.
Imeandaliwa na kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako